Mafuriko Kenya: KHRC yawashtaki mawaziri watatu kwa uzembe

Tume ya Haki za Binadamu nchini Kenya (KHRC) imethibitisha siku ya Ijumaa kuwa imewashitaki maafisa watatu wa serikali kwa uzembe na kushindwa kuwalinda waathirika wa mafuriko nchini humo.

Kelly Malenya, wakili wa KHRC, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba waliwasilisha kesi hiyo mahakamani siku ya Ijumaa na kwamba wamewashtaki Kithure Kindiki Waziri wa Mambo ya Ndani, Soipan Tuya waziri wa Mazingira na Alice Wahome waziri wa Ardhi.

Mwanasheria mkuu Justin Muturi ni miongoni mwa watu wanaohusishwa pia katika kesi hiyo inayolikabili pia Shirika la Reli la Kenya na mashirika mengine kadhaa ya serikali. KHRC imesema baadhi ya madhila na vifo vingeweza kuepukika ikiwa mamlaka ya Hali ya Hewa ya Kenya (KMD) ingechukua hatua ya kutoa tahadhari ipasavyo.

Tume hiyo ya Haki za Binadamu imesema inapambania kupata waraka kutoka kwa mahakama hiyo, ili kuishinikiza serikali kutoa msaada wa haraka wa kibinadamu pamoja na fidia kwa wahanga wa  mafuriko hayo yaliyosababisha vifo vya watu karibu 257.

Mbali na idadi hiyo ya vifo, kulishihudiwa pia uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwa ni pamoja na maporomoko ya udongo, uchafuzi wa vyanzo vya maji na kadhalika. Kumeripotiwa pia mlipuko wa nne wa kipindupindu ambao umethibitishwa na shirika la misaada la Ujerumani Welthungerhilfe.

Malenya amesema: Msimamo wetu ni kwamba watendaji wa serikali walishindwa katika wajibu wao na hiyo ndiyo kesi tuliyoiwasilisha mahakamani.”

Soma pia: Visa vya kipindupindu vyaripotiwa Kenya kufuatia mafuriko

Kulingana na taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, mvua kubwa na mafuriko vinavyoshuhudiwa tangu mwezi Machi vimesababisha uharibifu mkubwa katika mataifa ya Kenya, Tanzania, Burundi, Somalia, Rwanda na maeneo mengine ya Afrika Mashariki.

Dhoruba wakati wa msimu wa mvua si jambo geni lakini mwaka huu, mvua kubwa zimeshuhudiwa kutokana na aina fulani ya mfumo wa hali ya hewa wa El NiƱo. Wataalamu wanasema mabadiliko ya hali tabianchi yamechochea pia hali hii ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *