Siku ya wapendanao ni sikukuu ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 14 Februari ya kila mwaka (Valentine’s Day).
Historia yake imeanzia karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo Padri Valentine ambaye akaja kuheshimiwa kama mtakatifu hasa tarehe hiyo.Hadithi zilizosababisha sikukuu kuenea zaidi duniani kote.
Kwa mujibu wa mtandao wa history.com umeeleza kuwa kiongozi (Kaisari) wa kipindi hicho alikuwa Claudius II. Ambaye aliweka sheria kwa maaskari wote kutooa wala kufunga ndoa kwani aliamini askari mkakamavu ni yule asiyeoa wala kuwa na familia (kapera). Hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari.
Padri Valentine alipinga sheria hiyo, hivyo kuendelea kufungisha ndoa kwa siri. Mfalme Claudius II alipopata habari hizi aliamuru Valentinus akamatwe na anyongwe.
Padri Valentine aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu za kwanza za Valentine kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani, mwisho wa barua alihitimisha kwa maneno haya: “Kutoka kwa Valentine wako”.
Toka hapo Valentinus anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa karibia duniani kote.
KUENEA KWAKE DUNIANI:
Kwa kirumi ni siku ya kumbu kumbu (memoria day) na sehemu nyingine ni (festum) maana yake siku kuu ya daraja la kwanza kwa kumkumbuka Padri Valentine aliyeuawa na utawala wa kirumi sababu ya kutetea waumini wake kufunga ndoa badala ya kuishi na vimada tu.Lakini sikukuu hiyo ikaenea sana katika nchi za magharibi na baadaye karibia sehemu kubwa ya ulimwengu na kuisherehekea kama siku ya wapendanao kinyume cha dhamira ya Mt. Valentine.
Watawala wa dola ya kirumi walikuwa na fikra za kueneza dola ya kirumi duniani kote na hivyo vijana hawakutakiwa kuoa, ili wawe huru muda wote kwenda vitani kupigania nchi.Warumi waliamini vijana wangeoa/kuolewa wasingekuwa na uhuru wa kwenda vitani bali kuwa na famiia zao. Vijana wengi wakawa na mtindo wa kuwa na vimada tu kitu ambacho kanisa lilikukwa linapinga.
Padri Valentine ambaye alikuwa Roma akawa anawahimiza vijana kufunga ndoa badala ya kufanya ngono bila ndoa kwani ni dhambi na kitu kisichokubalika mbele ya Mungu.Akawa anafungisha ndoa kwa siri kwenye makatakombe (mahandaki chini ya kanisa ambako kuna sehemu za ibada kwa watu wachache), alifanya hivyo kwa vile kufunga ndoa hadharani ilikuwa ni kukiuka amri ya wakuu wa dola ya kirumi.
Baadhi ya watu walifichua siri hiyo, hivyo Padri Valentine alishikwa na dola ya Warumi na kuuawa kama shahidi mfia dini kwa ajili ya kutetea waumini wake wafunge ndoa ili waache maisha ya ngono zembe.
Wakristo wakaweka siku ya kumkumbuka Padri Valentine kama mfia dini, sababu ya kutetea maisha ya wanakanisa kuwa wanandoa.Sikukuu ikaenea katika makanisa ya nchi za magharibi na hata duniani ambako wanakanisa wanamkumbuka Mt. Padri Valentin.
Baadaye ikapokelewa na watu hata wasio na imani ya kikristo kama ni siku ya kumbu kumbu ya Mt. Valentine kama mtetezi wa Ndoa.Maudhui ya siku hiyo kwa wasiowanakanisa imechukua maana nyingine ya kwamba ni siku ya wapendanao, hata kwa wasio wanandoa bali mradi wanapendana, kitu ambacho ni kinyume cha malengo ya mfia dini Mt. Padre Valentin aliyetaka vijana wafunge ndoa.